Jumanne 3 Novemba 2026 - 17:00
Wanawake wana nafasi muhimu katika kuendeleza Muqawama kupitia malezi ya kizazi chenye msimamo wa kupinga dhuluma

Hawza/ Al-Mousawi, akisisitiza nafasi kuu ya wanawake katika safu ya Muqawama, amesema kuwa; kulea kizazi chenye msimamo wa kupinga dhuluma, kuimarisha misingi ya familia na kuhamishia utamaduni wa kusimama imara kwa vizazi vijavyo ni miongoni mwa mambo muhimu zaidi yanayochangia kuendeleza mapambano dhidi ya ubeberu wa kimataifa.

Kwa mujibu wa mwandishi wa Shirika la Habari la Hawza kutoka Mashhad Iran, Huda al-Mousawi, mwanaharakati wa masuala ya utamaduni kutoka Lebanon, siku ya Jumatatu, tarehe 11 Aban, katika jopo la tano la Mkutano wa Kimataifa wa Kupinga Ubeberu katika Fikra za Kiongozi Shahidi wa Mapinduzi, lililokuwa na mada isemayo: Nafasi ya malezi ya akina mama, uimara wa familia na uhusiano wa wananchi na uongozi katika kuimarisha Muqawama na kuendeleza uwepo katika medani, lililofanyika katika ukumbi wa Sheikh Tabarsi wa Taasisi ya Utafiti wa Kiislamu ya Haram ya Imam Ridha (as), alisisitiza nafasi ya wanawake katika kuendeleza harakati za kishujaa za medani na mitaani, kuimarisha uwezo wa jamii wa kustahimili changamoto, pamoja na nafasi yao kuu katika kulea kizazi chenye msimamo wa Muqawama, kuimarisha misingi ya familia na kudumisha msimamo imara dhidi ya ubeberu wa kimataifa.

Alisema: «Mwanamke ni sehemu muhimu ya mapambano dhidi ya ubeberu, kwa sababu, mbali na kushiriki katika medani ya mapambano, analea kizazi chenye msimamo wa Muqawama na kupitia mchango wake, huwaelekeza pia wanafamilia wengine katika njia ya Muqawama na kusimama imara».

Al-Mousawi, akitoa salamu za rambirambi kufuatia siku za kumbukumbu ya kuuawa kkshahidi Bibi Fatimah Zahra (as), alielezea kuwa kuwepo katika jirani ya Haram tukufu ya Imam Ridha (as) ni fursa yenye thamani kubwa. Aidha, akimkumbuka Kiongozi Shahidi wa Mapinduzi ya Kiislamu (ra), aliongeza: «Aliendelea kuinua bendera ya Ahlul-Bayt (as) na kutumia uwezo wake wote katika kulinda njia hii».

Alielezea kuwa fikra za Kiongozi Shahidi kuhusu kupinga ubeberu zilitokana na misingi ya kidini, kiitikadi na Qur'ani, na kusema: «Msimamo wake katika kukabiliana na ubeberu wa kimataifa ulikuwa wazi kabisa, na alijitahidi kuubadilisha wito wa kupambana na utawala wa mabavu na kuufanya kuwa utamaduni wa jumla na mapambano yenye utambuzi miongoni mwa mataifa».

Mwanaharakati huyo wa masuala ya utamaduni kutoka Lebanon, akizungumzia kauli mbiu ya “Mauti kwa Marekani”, alisisitiza: «Kauli mbiu hii ilikuwa na ujumbe wa kuyaamsha mataifa na kuyatambua kuhusu jinai za ubeberu wa kimataifa; jinai ambazo leo hii tunashuhudia mifano yake iliyo wazi huko Palestina na Ghaza».

Hizbullah imesimama kidete dhidi ya sera za uchokozi za utawala wa Kizayuni

Dada wa Shahidi Sayyid Abbas Mousavi, akizungumzia mashambulizi ya utawala wa Kizayuni dhidi ya Lebanon, alisema: «Kubomoa nyumba, kulipua majengo na kuwaua wananchi ni miongoni mwa sura za tabia za kinyama za utawala wa Kizayuni, ambazo wananchi wa Lebanon pia wamezipitia. Hata hivyo, Hizbullah imesimama kidete dhidi ya vitendo hivyo».

Alizitaja juhudi za kuinyang'anya Hizbullah silaha zake na kuyachochea makundi ya kidini dhidi ya mkondo wa Muqawama na Waislamu wa Kishia kuwa miongoni mwa hatua nyingine zinazochukuliwa dhidi ya safu ya Muqawama. Aidha, akizikosoa sera za serikali ya Lebanon, alizitathmini sera hizo kuwa zinaendana na matakwa ya utawala wa Kizayuni.

Mwanaharakati huyo wa masuala ya utamaduni kutoka Lebanon alisisitiza: «Sisi tumesimama kwa dhamira na imani kwa ajili ya kuhifadhi Muqawama na umoja wa Kiislamu. Subira yetu katika kukabiliana na adui ni subira ya kimkakati. Tunaiona misimamo hii ya kusimama imara kuwa inaendeleza mwongozo wa Kiongozi Shahidi katika njia ya kukabiliana na ubeberu wa kimataifa».

Mfano wa Fatimiyyah ndio msingi wa mchango wa wanawake katika safu ya Muqawama

Akizungumzia ushiriki wa wanawake nchini Palestina, Yemen na Iran, alibainisha: «Mfano wa Fatimiyyah umejitokeza katika namna wanawake wanavyotekeleza majukumu yao leo hii. Hawa ni wanawake ambao wapo katika medani pamoja na wanaume na wanachukua jukumu la kukabiliana na matatizo na changamoto mbalimbali».

Al-Mousawi, akieleza kuwa nafasi ya wanawake katika kulea kizazi chenye msimamo wa Muqawama imewafanya kuwa miongoni mwa walengwa wa ubeberu, alikumbusha: «Mwanamke, kwa kutumia elimu, kalamu na uwezo mwingine alionao, anashiriki katika Jihadi kubwa na ana mchango mkubwa katika kuendeleza njia ya Muqawama».

Akizungumzia ufafanuzi wa mifano miwili ya mwanamke wa Kufa na mwanamke wa Karbala katika kauli za Kiongozi Shahidi, aliendelea kusema: «Mfano wa mwanamke wa Karbala ni mfano wa Muqawama, subira na kuwahamasisha wengine kusimama imara. Katika mfano huu, mwanamke, mbali na juhudi zake za kujitolea na kutekeleza majukumu yake, pia analea kizazi kitakachoshiriki katika medani na kutetea tunu na maadili».

Mwanaharakati huyo wa masuala ya utamaduni kutoka Lebanon, akirejelea msisitizo wa Imam Khomeini (ra) kuhusu nafasi ya wanawake katika ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, alieleza kuwa ushiriki na uwepo wao katika mabadiliko ya kijamii na kusimama imara dhidi ya dhuluma ni jambo la lazima.

Al-Mousawi aliishukuru Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa namna ilivyoandamana na Muqawama wa Lebanon, pamoja na wananchi wa Iran, akisema: «Wananchi na viongozi wa Iran wamesimama pamoja na Muqawama katika nyanja za kijeshi na kidiplomasia, na pia wametoa makamanda na wapendwa wao katika njia hii».

Akizishukuru juhudi za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran za kuhakikisha suala la Lebanon linajumuishwa katika makubaliano na kufuatilia juhudi za kumaliza vita nchini humo, alisema: «Sisi tumesimama pamoja nanyi, tukiwa tumeshikana mikono, na tutaendelea kudumisha mshikamano na muungano huu».

Mwanaharakati huyo wa masuala ya utamaduni kutoka Lebanon, akisisitiza kauli mbiu ya «Hayhata Minna al-Dhillah» (Uwe mbali nasi udhalili), aliuelezea msimamo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran dhidi ya ubeberu kuwa umetokana na Madrasah ya Imam Hussein (as), na kubainisha: «Pamoja na kujitolea kote na mashahidi wote tuliowatoa, bado tutaendelea kusimama imara katika njia ya Muqawama».

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha